Habari

Imewekwa: Oct, 06 2018

Mradi wa Maji Ukalawa-Mkandarasi na Mhandisi Wapewa Muda Kueleza Sababu za Mradi Kukwama

News Images

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) leo ametoa muda wa saa kumi na mbili (12) kwa Mkandarasi, pamoja na Mhandisi wa maji aliyesimamia mradi wa maji wa Ukalawa mkoani Njombe kueleza sababu za kukwama kwa mradi huo ambao serikali imeshalipa fedha.

Mhe. Aweso (Mb) ambaye ameanza ziara ya kikazi mkoani Njombe ya kukagua mradi kwa mradi inayohusu sekta ya maji amesema itakapofika saa mbili kasoro asubuhi, tarehe 06.10.2018 wahusika hao wakutane nae katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe bila kukosa, kabla ya kutafutwa.

Mhe. Aweso (Mb) ameainisha kuwa kumbukumbu zinaonyesha mkandarasi aliyepewa kandarasi ya mradi huo wenye thamani ya shilingi Milioni 562, tayari ameshachukua malipo kiasi cha Shilingi Milioni 532 wakati wananchi bado hawapati majisafi na salama kama serikali ilivyopanga.

Mhe. Aweso (Mb) akiongea na wananchi wa vijiji vya Ukalawa na Kitole ambao wanategemea majisafi na salama kutoka katika mradi huo amesema serikali ikitoa fedha maana yake ni wananchi kupata huduma ya maji, na si vinginevyo, na suala la kuoneana haya katika kazi halina nafasi kwasababu maji hayana mbadala.

Mhe. Aweso (Mb) amewakumbusha wataalam wa maji kuwashirikisha wananchi katika miradi ya maji ili wajue kazi inavyofanyika, pia kulinda miradi hiyo. Mradi wa maji Ukalawa una vituo vya maji 13 ambavyo havitoi maji.

Huduma ya majisafi na salama kwa Mkoa wa Njombe ni asilimia 55.7 kwa mjini na asilimia 65.5 vijijini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Maji na Umwagiliaji

05.10.2018