Habari

Imewekwa: Oct, 06 2018

Mradi wa Maji Ukalawa-Kitole Wawafikisha Wahusika Polisi

News Images

Kutokua makini katika uratibu, usimamizi na ujenzi wa mradi wa maji mkoani Njombe kumewaweka matatani baadhi ya watendaji wa serikali na wakandarasi waliopewa dhamana ya kujenga na kufikisha majisafi na salama kwa wananchi.

Mradi uliotiliwa shaka wa Ukalawa na Kitole umesubiriwa na wananchi kwa zaidi ya miaka mitano na bado umekua butu kukidhi kiu ya wakazi wa vijiji vya Ukalawa na Kitole. Mradi huo umejengwa na kampuni ya Kihanga Farm International iliyolipwa kiasi cha Shilingi Milioni 532 kati ya Shilingi Milioni 562.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza wahusika walioshiriki katika mradi huo wakiwamo Watalaam wa maji wa Serikali popote walipo, Mhandisi Mshauri wa mradi na Mkandarasi wa mradi wasaidie Jeshi la Polisi kupata undani wa taarifa zinazohusu mradi, ikiwamo malipo yaliyofanyika wakati wananchi hawapati maji.

Mhe. Aweso (Mb) katika kikao kilichodumu kwa saa sita kilichowakutanisha watalaam wa maji, na baadhi ya walioshiriki katika ujenzi wa mradi wa maji Ukalawa-Kitole, amesema miradi ya maji sio kichaka cha kupitisha fedha na kusisitiza endapo mhusika yoyote atabainika kushiriki kuhujumu mradi huo, hata kama amestaafu utumishi wa umma, atatafutwa popote alipo na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Baada ya kikao kumalizika baadhi ya wahusika kutoka kampuni iliyopewa kandarasi ya Kihanga Farm na wataalam wa maji wa serikali walioshiriki walikabidhiwa kwa vyombo husika ili kusaidia zaidi kwa taarifa muhimu.

Mhe. Aweso (Mb) amesema hakuna faida ya kuwa na mtalaam wa maji anayekabidhiwa mradi bila kujiridhisha na ubora wake kama taratibu zinavyotaka, ambapo imebainika moja ya udhaifu katika mradi wa maji Ukalawa-Kitole ni kwenda kinyume na mkataba, na kutozingatia ushauri wa Mhandisi Mshauri wa mradi na kubadili mfumo wa kusukuma maji kutoka wa kutumia jenereta, kwenda mfumo wa kutumia nishati ya jua (solar) wakati mazingira ya mradi sio rafiki kwa mfumo wa nishati ya jua.

Mhe. Aweso (Mb) ameagiza kutokana na udhaifu ulioonekana katika mradi huo ameagiza timu aliyoiunda akiwa mkoani Mbeya mwezi Oktoba 2018, ipite katika mradi wa maji Ukalawa na mradi wa Lugenge ambao madakio ya maji mawili yamekamilika lakini mradi bado hauridhishi na ukiwa katika asilimia 60 ya kazi pamoja na Mkandarasi kuongezewa muda.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Maji na Umwagiliaji

06.10.2018