Habari

Imewekwa: Sep, 13 2018

Mkutano Wa Sita Wa Kamati ya Kitaifa ya Wadau wa Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi Wafanyika Dodoma

News Images

Mkutano wa wadau kuhusu majadiliano ya utekelezaji wa maandalizi ya Mpango Mkakati wa Bonde la Mto Zambezi (Zambezi Watercourse Commission Strategic Plan) umefanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Maji, jijini Dodoma.

Lengo ya mkutano huo likiwa ni kupitia rasimu ya mkakati ili kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanajumuishwa katika mpango huu, ambao unategemewa kutekelezwa katika vipindi vya mwaka 2018-2027 na 2028-2040.

Mkutano huo umeenda sanjari na Mkutano wa sita wa Kamati ya Kitaifa ya Wadau wa Bonde la Mto Zambezi, ukifuatia mkutano wa tano wa Kamati ya Kitaifa uliofanyika Agosti, 2018 jijini Mbeya. Kamati hii iliundwa mwaka 2011 na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Sekretariati ya Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (Zambezi Watercourse Commission Secretariat).

Lengo la kamati hiyo ni kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Bonde la Mto Zambezi katika ngazi ya Kitaifa kwa ajili ya utekelezaji, pamoja na kushiriki na kuiwakilisha nchi katika matukio mbalimbali ya Kikanda yanayohusu Bonde la Mto Zambezi.

Baadhi ya malengo mengine ya kamati hiyo ni pamoja na; kuetetea maslahi ya nchi yetu na kuendeleza ushirikiano wa Kimataifa katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika Bonde la Mto Zambezi, kuwa kiunganishi kati ya Sekretariati ya ZAMCOM pamoja na wadau wa Kitaifa na kushauri nchi kuhusu mipango, usimamizi, matumizi, uendelezaji na uhifadhi wa maji ya Bonde la Mto Zambezi.

Mkutano huo umeshirikisha Wizara ya Maji, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Nyasa, Wizara ya Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo, Sekretarieti za Mikoa ya Ruvuma na Njombe, Halmashauri za Wilaya za Kyela, Makete, Ludewa na Nyasa na Tanzania Water Partnership (TWP).