Habari

Imewekwa: Nov, 13 2018

Mji wa Longido Kupata Majisafi na Salama kwa Asilimia 100

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) amesema hali ya upatikanaji majisafi na salama katika mji wa Longido wenye idadi ya wakazi 16, 712 inaongezeka kutoka asilimia 15 ya sasa inayowafikia wananchi 2, 510 hadi kufikia asilimia 100.

Waziri Mbarawa akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huoamefafanua kuwa hatua hiyo inamaanisha wananchi wote katika mji huo watapata huduma ya majisafi na salama kupitia mradi mkubwa wa maji wa Longido unaoanzia mto Simba katika wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha Mita za ujazo 2,160 kwa siku wakati mahitaji halisi katika mji wa Longido ni Mita za ujazo 1,462.

Waziri Mbarawa ameainisha mradi wa maji Longido unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 15.7 tayari mabomba yenye urefu wa kilometa 94 yamelazwa kutoka katika chanzo cha maji cha mto Simba wilayani Siha na mkandarasi kampuni ya ujenzi ya STC anatakiwa kukabidhi mradi mwezi ujao Tarehe 15 Desemba 2018.

Waziri Mbarawa amesema ili kuhakikisha wananchi wa Longido wanapata maji huduma ya maji haraka na kujikita katika shughuli nyingine za maendeleo, Serikali iliamua kandarasi ya mradi huo itekelezwe na Wakandarasi waliopewa kazi tofauti; kazi hizo ni pamoja na kujenga matanki, ujenzi wa mifumo ya kusambaza maji, na ujenzi katika chanzo cha maji.

Waziri Mbarawa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama kama ambavyo Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inavyoelekeza kuwapatia wananchi waishio vijijini majisafi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Aidha, ameongeza nia hasa ni kufanikisha asilimia 85 ya wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2020 na asilimia 95 katika miji. Pamoja na hilo amewataka wananchi kutunza mazingira na kuotesha miti kulinda vyanzo

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Novemba 13, 2018.