Habari

Imewekwa: Feb, 11 2019

Mamlaka za Maji Nchini Zatakiwa Kufanya Kazi kwa Uadilifu

News Images

Waziri wa Maji, Mh. Profesa Makame Mbarawa amezitaka Mamlaka za Maji nchini kufanya kazi kwa uadilifu na kujiendesha kibiashara ili kuachana na zana ya kutegemea fedha au ruzuku kutoka Wizarani. Kwa muda mrefu Mamlaka zimekuwa zikitegemea fedha kutoka Wizarani kwa ajili ya kulipia bili za umeme.

Mamlaka zibadilike zifanye kazi kibiashara, ziongeze mindao ya maji kwa wananchi ili wananchi wapate majisafi na salama na zenyewe zijiongezee makusanyo.

“Katika kipindi changu biashara ya kutegemea kupata asilimia 25 ili kulipia gharama za uendeshaji haipo” alisema Waziri.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo alipoanza ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maji inayosimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA).

Akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), wafanyakazi wa ofisi ya Bonde la Kati na wa Maabara ya Maji Singida, Profesa Mbarawa aliwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuongeza makusanyo na kuzifanya Mamlaka zao zijisimamie na kuongeza hata mishahara yao.

“Uadilifu ni jambo muhimu sana, heshima inapanda na mambo yanakuwa mazuri endapo mtakuwa waadilifu” alisema Waziri.

Aidha, alisema suala la uadilifu linapaswa kuwa kwa watumishi wote viongozi na watendaji wengine na pia ushirikishwaji wa maamuzi kwa watumishi ni jambo muhimu sana.

Wakati huo huo, Waziri aliwataka Wenyeviti wa Bodi za Maji Nchini kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Paskasi Muragili alimshukuru sana Waziri kwa kuja Singida kukagua miradi ya Maji na kuona changamoto zilizopo. Aidha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida Bw. Ahmed Athuman naye alitoa shukrani nyingi kwa Waziri.