Habari

Imewekwa: Dec, 20 2018

MAMLAKA YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MJINI MOSHI YAIBUKA KINARA

News Images

TAARIFA YA UMMA

PONGEZI KWA MAMLAKA YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MJINI MOSHI KWA KUWA MAMLAKA BORA YA MAJI AFRIKA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA

Mamlaka ya Maji Safi na USafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) imekuwa mshindi wa jumla (overall winner) kati ya mamlaka nane (8) zilizoshindanishwa na Jumuiya ya Taasisi za Udhibiti wa Sekta ya Maji zilizopo katika nchi za mashariki na kusini mwa Afrika (ESAWAS). Jumuiya hii inaundwa na wanachama nane kutoka katika nchi za Kenya, Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Lesotho, Zambia, Burundi na Zanzibar.

Katika mchakato huu Taasisi ya ESAWAS ilishindanisha Mamlaka moja bora kutoka kila nchi wanachama na kupata mshindi wa jumla kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017. Kwa Tanzania mamlaka bora katika kutoa huduma ya maji mwaka 2016/2017 ilikuwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA). ESAWAS hutumia vigezo vitatu vifuatazo katika kushindanisha mamlaka za maji:

 • i.Ubora wa huduma (quality of service)
 • ii.Ufanisi wa kiuchumi (economic efficiency)
 • iii.Uendelevu wa mtoa huduma (operator efficiency)

Katika kikao cha Mkutano Mkuu (AGM) kilichofanyika tarehe 30 Novemba 2018, Taasisi ya ESAWAS iliitangaza rasmi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kuwa Mshindi wa jumla kwa kupata 79.9%, ikifuatiwa na WASAC ya Rwanda kwa 77.4%, na Nyeri ya Kenya iliyopata 70.8%. Aidha, MUWSA imekuwa mshindi wa kwanza katika eneo la uendelevu wa huduma kwa kupata 94.6%, na mshindi wa pili katika eneo la ubora wa huduma kwa kupata 87.5%. Washindi wengine katika maeneo mbalimbali ni kama ifuatavyo:

 • i.Ubora wa huduma (quality of service)
 • a)Mshindi wa kwanza: WASAC –RWANDA (88%)
 • b)Mshindi wa pili: Moshi WSSA-Tanzania na Nyeri -Kenya (87.5%)
 • c)Mshindi wa tatu:Southern –Zambia (84.1%)
 • ii.Ufanisi wa kiuchumi (economic efficiency)
 • a)Mshindi wa kwanza: WASAC –RWANDA (91%)
 • b)Mshindi wa pili Moshi: WSSA-Tanzania (53.8%)
 • c)Mshindi wa tatu: Southern –Zambia (52.6%)
 • iii.Uendelevu wa mtoa huduma (operator efficiency)
 • a)Mshindi wa kwanza: Moshi WSSA-Tanzania (94.6%)
 • b)Mshindi wa pili: Nyeri: Kenya (66.7%)
 • c)Mshindi wa tatu: WASAC –RWANDA (50%)

Tunawapongeza MUWSA kwa kazi nzuri katika kutoa huduma ya maji Mjini Moshi. Tunaamini ushindi huu utakuwa kichocheo kwa mamlaka zingine za maji kuongeza juhudi katika kutoa huduma ya maji nchini.

Imetolewa na

Prof. Kitila Mkumbo

KATIBU MKUU

WIZARA YA MAJI

20 Desemba 2018