Habari

Imewekwa: Jul, 04 2018

LENGO LETU NI KUPELEKA MAJI KWA WATANZANIA-PROF. MBARAWA

News Images

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Makame Mbarawa amesema lengo la Serikali ni kupeleka maji kwa watanzania ambao wengi wao wanakosa huduma hiyo maeneo ya mijini na vijijini, na kwa kufanya hivyo maisha ya watanzania wengi yatabadilika kwa kupata huduma hiyo.

Amesema hayo alipofanya ziara katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji za DAWASA na DAWASCO kwa lengo la kufuatilia maendeleo na utendaji wa taasisi hizo.

‘‘Bado maeneo mengi nchini hayana maji, wapelekeni huduma hii kwa sababu hatuna sababu ya msingi ya kutofanikisha jambo hilo. Tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kubadilisha maisha ya watanzania kwa kuwapatia huduma ya maji ya uhakika. Niwahakikishieni tutafuatilia hatua zote za utekelezaji wa miradi yote ya maji, ni lazima ikamilike kwa wakati na tuone thamani halisi ya fedha zinazotumika’’, amesema Prof. Mbarawa.

‘‘Nyinyi kama DAWASA na DAWASCO mna dhamana ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji kwenye maeneo yenu na miundombinu yake; na hakikisheni mnaongeza wateja, mnamaliza tatizo la upotevu wa maji na kukusanya mapato vizuri ili muweze kufanya shughuli zenu kwa ufanisi, alisisitiza Prof. Mbarawa.

Wakati huo, Prof. Mbarawa amesema kuwa lengo la Serikali la kuziunganisha taasisi hizo si kuwaumiza watumishi, bali ni kuwa na taasisi moja yenye nguvu na ufanisi kiutendaji ili kutimiza lengo la kutoa huduma bora ya maji.Huku akisisitiza mchakato huo hautachukua muda mrefu kukamilika, hivyo watumishi hao wawe wavumilivu.