Habari

Imewekwa: Sep, 22 2018

Kero ya Maji Matala Kufikia Kikomo

News Images

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ameagiza wataalamu kutoka Bonde la Rukwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi ili kubaini kiasi cha maji kilichopo katika Kijiji cha Matala, wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa ambayo yatatumika kama chanzo cha maji kwa mradi wa Matala.

Ametoa kauli hiyo alipotembelea mradi huo mara baada ya kupata taarifa kuwa tangu utekelezaji wake uanze mwaka 2013 bado haujaanza kutoa maji na kusababisha tatizo la maji kijijini hapo.

Mradi huo umeonekana ukiwa na kasoro ya mabomba kupasuka na kukosa chanzo cha maji cha uhakika, pamoja na kuwepo kwa mfumo wa kusambazia maji kwa wananchi.

Akitoa maagizo kwenye mkutano wa hadhara mbele ya wakazi wa Matala, Profesa Mbarawa amewataka wataalamu kutoka Bonde la Ziwa Rukwa kutafiti chanzo cha maji cha chini ya ardhi na kumpa taarifa haraka.

’’Nataka muanze kazi ya kutafiti maji chini ya ardhi eneo la Matala mara moja na baada ya kupokea taarifa yenu, nitawatuma Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) waje kuchimba kisima ili maji yaanze kusambazwa kwa wananchi kwa sababu mfumo wa usambazaji upo ili ndani ya miezi miwili ijayo huduma ya maji iwepo ’’, alisema Profesa Mbarawa.

‘‘Ikibainika kuwa mabomba yaliyowekwa yako chini ya kiwango, hatutamlipa mkandarasi kwa sababu ni kinyume na makubaliano yetu kimkataba na hilo niwaambie ukweli nitalifuatilia mpaka nijiridhishe kabla ya kufanya malipo ya hati yake ya madai’’, alisisitiza Profesa Mbarawa.

Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy amemshukuru Profesa Mbarawa kwa kuwa waziri wa kwanza kufika katika Kijiji cha Matala kuja kujionea kero ya maji waliyonayo na hatua alizochukua kwa nia ya kumaliza tatizo hilo kwa wananchi wa kijiji hicho. Lakini pia, alimshukuru kwa kukubali ombi lake la kuleta wataalamu na kutafuta chanzo kipya cha maji ambacho kitazalisha maji ya kutosha.

Profesa Mbarawa amekamilisha ziara yake ya siku tatu mkoani Rukwa kwa kutembelea wilaya za Sumbawanga Mjini, Sumbawanga Vijijini, Kalambo na Nkasi ambapo alikagua ujenzi wa miradi ya maji na kusikiliza kero za wananchi.