Habari

Imewekwa: Oct, 10 2018

Jiji la Arusha Kupata Huduma ya Maji kwa Asilimia 100 Mwaka 2020

News Images

Jiji la Arusha linategemea kuwa na huduma ya majisafi na salama kwa kiwango cha asilimia 100 ifikapo mwaka 2020 mara baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kutia saini mkataba wa zaidi ya Shilingi Bilioni 520 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji.

Mkataba huo unahusisha utekelezaji wa mradi wenye lengo la kuongeza huduma ya usambazaji wa majisafi na salama kutoka44% ya Jiji la Arusha hadi kufikia 100%na kutoa huduma ya majisafi na salama kwa baadhi ya maeneo ya wilaya za Arumeru na Hai ambazo zinapitiwa na mradi huo.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imeamua kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika jiji la Arusha ili kuondoa kero ya upungufu wa majisafi na uondoaji majitaka katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Arusha.

Amesema mradi huu wa kuboresha huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira umelenga kulifanya Jiji la Arusha kuwa na hadhi inayostahili, ukizingatia ndio kitovu cha utalii Tanzania na Afrika kwa ujumla, maarufu kama Geneva ya Afrika. Utekelezaji wake utafanywa na wakandarasi watatu wa kampuni za Sinohydro Corporation Ltd, Tanchi Brother Construction Co. Ltd na Kiure Engineering Limited kila mmoja akiwa na sehemu yake ya kazi.

Profesa Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali imechukua hatua hiyo kutokana na upungufu uliopo katika Jiji la Arusha, ambapo kwa sasa mahitaji yake ni lita milioni 94 kwa siku na kiwango cha uzalishaji kwa sasa ni lita milioni 45, wakati mradi ukikamilika utazalisha lita milioni 200 za maji kwa siku na kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji.

Mradi huu unategemea kukamilika ifikapo Juni, 2020 nautakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 827,923 wa kata zote za Jiji la Arusha, 155,222 wa baadhi za kata za Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na baadhi ya maeneo ya wilaya za Arumeru na Hai kulipo vyanzo vya maji vya mradi huo hadi kufikia 2030.

Mkurugenzi wa AUWSA ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi huo, Mhandisi Ruth Koya ameishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha wakazi wa Jiji la Arusha na kusaidia upatikanaji wa fedha hizo nyingi za utekelezaji wa mradi huo, ili kuboresha huduma ya usafi wa mazingira ndani ya Jiji la Arusha na kuahidi kusimamia wakandarasi ipasavyo kulingana na matakwa ya mkataba wakizingatia thamani ya fedha.

Kazi za mradi huo zitahusisha ujenzi wa mashine za kusukuma maji kutoka kwenye visima, bomba kubwa za kusafirisha majisafi, bomba za upanuzi wa mtandao wa majisafi (Distributions Lines), mashine za kusukuma maji (Booster Pump Stations), matenki ya kuhifadhia maji, mfumo wa kieletroniki wa kuchukua taarifa (Intergrated Monitoring System) na jengo la ofisi za AUWSA.