Habari

Imewekwa: Oct, 24 2018

Hakuna Sababu Miradi ya Maji Isifanye Kazi-Profesa Mbarawa

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa amesema hatakubaliana na sababu yoyote ya miradi ya maji kutokufanya kazi, ni lazima hatua zichukuliwe kumaliza changamoto zote ili wananchi wapate majisafi na salama.

Ametoa kauli hiyo wakati akiwe kwenye ziara ya kukagua miradi ya maji katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma kwa lengo la kujionea utekelezaji wake.

Akiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Isabella Chilumba na timu ya wataalamu kutoka mkoa wa Ruvuma, Bonde la Ziwa Nyasa na Halmashauri, Profesa Mbarawa ametembelea mradi ya Ukuli-Kingerikiti ambao umekuwa ukisusua kwa miaka sita tangu uetekelezaji wake uanze.

Ambapo iligundulika kuwa maji yanayosafirishwa na bomba kuu kutoka kwenye chanzo, hayafiki kwenye tenki kutokana na viunganisho vya bomba kupasuka kutokana na msongo wa maji yanayopita kwenye bomba hilo.

Akionyeshwa hali ya kukerwa na hali hiyo Profesa Mbarawa amemwagiza Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Songea (SOUWASA), Mhandisi John Kapinga na Mhandisi wa Mkoa wa Ruvuma, Genes Kimaro pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kutafuta ufumbuzi wa tatizo linalosababisha mradi huo kukwama.

Profesa Mbarawa amesema anataka wataalamu hao wafike katika mradi huo na kufanya utafiti utakaoleta ufumbuzi wa changamoto hiyo na kuishauri wizara hatua ya kuchukua ili uanze kufanya kazi.

Aidha, akiwa kwenye mradi wa Litindoasili-Lumecha ambapo amejionea mradi huo ukiwa changamoto ya huduma ya maji inayopatikana kutotosheleza licha ya mradi huo kugharimu takribani Shilingi Milioni 361.

Profesa Mbarawa ametaka kitafutwe chanzo kingine cha uhakika, kitakachokuwa endelevu ili kiweze kutumiwa na mradi huo na wakazi wa vijiji hivyo wapate majisafi na salama ya uhakika.

Akiwataka wananchi kijijini hapo kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa wataalamu katika utafiti wa chanzo kipya na kumaliza tatizo lao la maji.

Amesema lengo la ziara yake ni kutembelea miradi yenye changamoto kwa nia ya kuzitatua ili kumaliza kero ya maji kwa wananchi na kutimiza lengo la Serikali kuwapatia wananchi wake majisafi na salama.