Habari

Imewekwa: Dec, 06 2018

Dawasa Tatueni Kero za Wananchi kwa Wakati-Profesa Mbarawa

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ameitaka DAWASA kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati katika kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Profesa Mbarawa ametoa rai hiyo wakati akiwa ziarani katika maeneo ya Kimara kwa lengo la kusikiliza na kujionea kero za wananchi ambazo amekuwa akizisikia.

Akiwa katika mitaa ya Aseno na Saranga katika Kata ya Saranga, Kimara Temboni amezungumza na wakazi wa maeneo hayo na kuwataka wafike Ofisi za DAWASA za Kimara kwa wale wote ambao hawajaunganishiwa maji na wapewe huduma hiyo na kulipa taratibu baada ya kuanza kupata huduma hiyo.

Pia, amewataka watendaji wa DAWASA, hususani mameneja kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua kwa wakati, na sio kusubiri mpaka yeye mwenyewe afike kufanya hivyo.

Amesema ni wajibu wa DAWASA kuboresha huduma kwa wateja kwa kuwa mteja ni mfalme na anastahili huduma bora yenye kuridhisha.

Akisisitiza Serikali imedhamiria kuwa karibu na wananchi kwa kuwafuata na kusikiliza kero zao ili wazipatie ufumbuzi kwa wakati kwa kuwapatia huduma bora na ya uhakika ya maji.

Profesa Mbarawa amechukua maamuzi ya kumuondoa kazi Meneja wa DAWASA Ofisi za Kimara, Damson Mponjoli kutokana na kutoridhishwa na ufuatiliaji wake na hatua anazochukua kuhakikisha anamaliza kero za wakazi wa Kimara.

Profesa Mbarawa amesema ataendelea na zoezi la kufuatilia na kusikiliza kero za wakazi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuitaka DAWASA ifanye bidii kumaliza tatizo la maji kwenye kwa wananchi jijini Dar es Salaam.