Habari

Imewekwa: Nov, 07 2018

Bei za Maji Zipangwe kwa Kigezo cha Nishati Inayotumika

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), pamoja na vigezo vingine, kupanga bei za maji kulingana na aina ya nishati inayotumika kwa miradi mbalimbali.

Waziri Mbarawa amesema nishati hizo ni pamoja na nishati ya jua (solar power), mafuta ya dizeli na Umeme na kufafanua kuwa amebaini uwepo wa tofauti kubwa katika bei za maji kwa wananchi hasa wale wanaotumia vituo vya kuchotea maji (DPs) na wale waliounganishiwa majumbani.

Amesema wananchi wanaotumia vituo vya kuchotea maji wanatozwa kati ya shilingi 50 hadi 500 kwa ndoo sawa na shilingi 1,000 hadi 10,000 kwa mita moja ya ujazo, wakati kwa wananchi waliounganishwa majumbani wanalipa kati ya Shilingi 300 (mkoani Geita) hadi 1,600 (mkoani Dar es salaam) kwa mita moja ya ujazo.

Mhe. Mbarawa, pamoja na maagizo hayo, ameelekeza pia wananchi waliokaribu na vyanzo vya maji wapewe kipaumbele katika kupatahuduma ya maji kwa sababu wao ndio walinzi wa miundombinu ya maji.

Maagizo mengine aliyotoa Waziri Mbarawa ni kuhusu mkandarasi aliye na mradi zaidi ya mmoja na utekelezaji wa mradi huo upo chini ya asilimia 50 asipewe kazi nyingine hadi akamilishe miradi ya awali. Aidha, ameagiza Wizara ya Maji kuimarisha ufuatiliaji wa vibali vya wataalam kutoka nje na kuhakiki wataalam hao ambao sifa zao za kazi hazipatikani hapa nchini ili kuharikisha utekelezaji wa miradi.

Ameongeza kuwa Wizara ya Maji inaandaa viashiria vya kupima utendaji wa mamlaka za maji (KPI) kwa kila mwaka kwasababu baadhi ya mamlaka zimeonekana utendaji wake ukishuka mwaka hadi mwaka. Sanjari na hilo, Waziri Mbarawa amezitaka Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha zinafikia kiwango cha kimataifa cha upotevu wa maji kilihokubaliwa ambacho ni asilimia 20.

Awali, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) aliwataka watalaam hao kusimamia miradi ya maji kwa ukamilifu na wasisubiri viongozi kubaini kasoro katika miradi ya maji nchini.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Novemba 7, 2018.