SERIKALI KUHAMASISHA SEKTA BINAFSI KUSHIRIKI KATIKA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI

Imewekwa: Jul 09, 2018


TAARIFA KWA UMMA

Tunapenda kuujulisha umma kuwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Washirika wa Maendeleo wa Sekta ya Maji wameandaa Kongamano maalum litakalowakutanisha Serikali na Sekta Binafsi ambao ni wadau wa Sekta ya Maji nchini.

Lengo la Kongamano hili ni kujadili fursa zilizopo na changamoto zinazoikabili sekta binafsi nchini katika kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya maji nchini. Malengo mahsusi ya kongamano hili ni pamoja na: kuhamasisha wakandarasi wa ndani kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya maji na kuhamasisha matumizi ya vifaa vya ndani katika ujenzi wa miradi na utoaji wa huduma ya maji kwa ujumla.

Kongamano hili litafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 20 Julai, 2018 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Washiriki 200 wanatarajia kuhudhuria Kongamano hili, wakiwemo Wakandarasi, Wazalishaji Viwandani, Wataalam Washauri na viongozi na maafisa wa serikali. Washiriki wengine ni wawakilishi kutoka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI); Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF); Shirikisho la Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA); Bodi ya Wasajili wa Wakandarasi (CRB); Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB); Jumuiya ya Biashara ya Wanawake nchini (TWCC); na Chama cha Wahandisi Washauri (ACET).

Mada mbalimbali zinatawasilishwa na kujadiliwa na na hatimaye kuandaliwa maazimio kwa ajili ya kufikishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi na utekelezaji. Matokeo tarajiwa ya kongamano hili ni pamoja na kuongeza idadi ya makampuni binafsi yanayoshiriki katika maendeleo ya Sekta ya Maji; kuongeza ubora wa kazi; na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini; .na kuongeza mchango wa Sekta ya Maji kwenye Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Prof. Kitila Mkumbo

Katibu Mkuu

Dodoma, 9 Julai 2018.