Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maji na Umwagiliaji Yatekeleza Agizo la Waziri Mkuu

Swahili

Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kufika Tunduru na kulipatia ufumbuzi tatizo la maji katika mji huo, alilolitoa siku chache zilizopita wakati alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Ruvuma. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameweza kufika Namtumbo kwa lengo la kujua changamoto zinazoikabili wilaya hiyo, ambapo kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 21 kwa sasa.Akizungumza katika ziara yake hiyo Aweso alisema kuwa kuna haja ya kuchukua hatua za haraka ili kuunusuru mji huo na hali mbaya iliyonayo, kwa kuipa nguvu miradi inayosuasua na kuahidi kutuma fedha mara moja ili kufanikisha jambo hilo.

‘‘Nitafanya utaratibu Sh. milioni 300 zinazohitajika zipatikane mwezi ujao, ili utekelezaji miradi inayosuasua ikamilike mara moja na wananchi waanze kupata maji kama Waziri Mkuu alivyoagiza kwani fedha ipo na ndio lengo letu kama wizara,’’ alisema Naibu Waziri. Pia, Aweso ameagiza wakandarasi kuacha visingizio na kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miradi kwa wakati kulingana na mikataba yao inavyoonyesha na si vinginevyo.

‘‘Umefika wakati wakandarasi kuacha visingizio ambavyo havina msingi wowote, nawaagiza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji nchi nzima wakamilishe miradi hiyo kwa wakati. Kama viwanda vya vifaa mbalimbali vipo nchini, wanunue vifaa katika viwanda hivyo na si kusingizia kuchelewa kwa vifaa kwa sababu vinaagizwa kutoka nje ya nchi, wakati hakuna sababu ya kufanya hivyo,’’ alisema Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri alitembelea Wilaya ya Tunduru ambapo hakuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo na kuagiza apate ripoti ndani ya siku tatu inayoeleza sababu za kusuasua kwa mmoja wa miradi wakati fedha zote za kutekeleza mradi huo zimeshalipwa na bado haujakamilika.

Photo: