Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Akutana na Balozi wa Uingereza

Swahili

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amekutana na Balozi wa Uingereza nchini Bi Sarah Cooke na kufanya mazungumzo ofisini kwake, Makao Makuu ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, mjini Dodoma kwa ajili ya kujadili changamoto katika sekta ya Maji. Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa kuangalia jinsi  serikali ya Uingereza inavyoweza kusaidia kuwezeshwa kujengwa kwa bwawa la Falkwa, nia ikiwa ni kutatua changamoto ya maji katika mji wa Dodoma ambao unatarajiwa kuwa na wakazi wengi kulinganisha na hapo awali.

Waziri ameiomba serikali ya Uingereza kusaidia ujenzi huo kutokana na umuhimu wake katika mji wa Dodoma ikizingatiwa kuwa Makao Makuu ya Serikali yamehamia hapa hivyo mahitaji ya huduma ya maji kuongezeka kwa kiasi kikubwa.  Aidha, Mhandisi Kamwele ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania kwa misaada mbalimbali inayotolewa kupitia Idara ya Maendeleo ya Kimataifa  (Department for International Development - DFID) katika kusaidia sekta ya Maji kupitia mfumo wa malipo kulingana na matokeo (Payment by Results).

Katika mazungumzo hayo ilibainika kuwa kasi matumizi ya fedha zinazotumwa katika Halmashauri nchini kupitia mfumo huo ni ndogo ukilinganisha na fedha zinazotumwa katika kutekeleza miradi ya maji. Hivyo Waziri amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliagiaji, Profesa Kitila Mkumbo kushirikiana na DFID kubaini changamoto na kuzitatua haraka iwezekanavyo.  Balozi amemuomba Waziri wa Maji kutatua changamoto zinazojitokeza ili kuweza kufanikisha malengo yaliyowekwa baina ya Serikali zao na kumuahidi Waziri Kamwele ushirikiano wa dhati katika kuinua sekta ya maji nchini ambapo mpaka sasa Serikali ya Uingereza imeshachangia kiasi cha Pauni  milioni 750 kusaidia jitihada mbalimbali za serikali za kuleta maendeleo. Ziara ya Balozi Cooke ilikuwa na lengo la kukutana na Waziri na kusikia vipaumbele vya Waziri kama kiongozi mwenye dhamana ya kuongoza Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Photo: