Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wataalamu wa AMCOW wakutana kujadili upatikanaji wa Maji ya uhakika kwa Bara la Afrika

Wataalamu wa Masuala ya Maji kutoka nchi 25 za Bara la Afrika wamekutana kujadili njia zitakazowezesha upatikanaji wa majisafi na salama mijini na vijijini kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030 barani Afrika. Mkutano huo umefunguliwa Jijini Dar es Salaam na Rais wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Nchi za Afrika (AMCOW) na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge ambaye amesema kuwa majadiliano hayo yametokana na Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 6 kuzitaka nchi zote ulimwenguni kuhakikisha kuwa wananchi wao wanapata huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

“Ili kuhakikisha agizo la Umoja wa Mataifa linatekelezwa, nchi wananchama za AMCOW ziliamua kuunda Kamati ya Wataalamu ya Ushauri (TAC) watakaojikita katika kupanga mipango na mikakati endelevu ili kuhakikisha utekelezaji wa agizo hilo,”alisema Inj. Lwenge. Waziri Lwenge ameongeza kuwa baada ya majadiliano hayo wataalamu hao watapeleka taarifa katika kikao kikuu cha Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika, kinachotegemewa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu mjini Abuja, Nigeria, ili kuweza kupata tathmini ya kila nchi inavyotekeleza azimio hilo. Aidha, Inj. Lwenge amefafanua kuwa kwa miaka mitano ijayo, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa wakazi wa mijini wanapata majisafi na salama kwa asilimia 95 na vijijini asilimia 85, uondoaji wa majitaka kwa asilimia 30 pamoja na kuhakikisha nyumba za vijijini zina vyoo vya kisasa ifikapo mwaka 2020.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa AMCOW, Dkt. Canisius Kanangire amesema kuwa kikao hicho kitakachochukua siku 5, kimewashirikisha wataalamu na wadau kutoka Mashirika mbalimbali yanayohusika na Wakuu wa Mabonde ya Maziwa na Mito Afrika ili nao waweze kutoa mchango wa mawazo utakaopelekea nchi za Afrika kuwa na maendeleo makubwa katika Sekta ya Maji.  ”Baraza la Mawaziri wa Maji kwa kushirikiana na wataalamu wa maji watawezesha utekelezaji wa mipango na mikakati mizuri ambayo itakayowezesha upatikanaji wa majisafi na salama kwa nchi zote za Afrika,” alisema Dkt. Kanangire.  

Dkt. Kanangire ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano inayoutoa kwa AMCOW  katika kuhakikisha inafanya kazi zake vizuri, hivyo anategemea kuwa kikao hicho kitatoa majibu ya uhakika wa utekelezaji wa mpango wa upatikanaji wa majisafi na salama kwa Bara la Afrika