Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Utangulizi

Mabonde ya Maji

Nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vya aina mbalimbali vya maji. Vyanzo hivyo ni: mito,Maziwa, Ardhi oevu na maji chini ya ardhi. Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeweka utaratibu wa usimamizi wa rasilimali za maji katika ngazi za mabonde ili kuweza kuleta usimamizi endelevu wa rasilimali hiyo.

Mfumo wa usimamizi wa rasilimali za maji kimabonde unalenga katika kuleta usimamizi thabiti na shirikishi unaowezesha kuleta usawa, ufanisi, na usimamizi endelevu wa rasilimali hiyo.

Mnamo mwaka 1989,kupitia sheria ya matumizi ya maji (kanuni na taratibu) kifungu namba 42 cha mwaka 1974, na marekebisho yake namba kumi ya mwaka 1981, Waziri mwenye dhamana ya maji alitangaza kwenye gazeti Mabonde Tisa ya Maji kwa madhumuni ya kuleta usimamizi bora wa rasilimali hiyo, Mabonde sita kati ya tisa ni ya kimataifa (Tunashirikiana na mataifa mengine).

Serikali ilianzisha Ofisi za Mabonde katika Bonde la Mto Pangani (1991), Bonde la Mto Rufiji (1993), Bonde la Ziwa Victoria (2000), Bonde la Wami/Ruvu (2001), Bonde la Ziwa Nyasa (2001), Bonde la Ziwa Rukwa (2001), Bonde la kati (2004), Bonde la Ziwa Tanganyika (2004), Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini (2004).
Kazi za Mabonde haya ni usimamizi wa rasilimali za maji, uchunguzi na uchimbaji wa maji chini ya ardhi, vilevile kuweka mipango na kufanya utafiti, usimamizi wa sheria na utunzaji wa mazingira ya vyanzo maji. Mabonde yanasimamiwa na maofisa mabonde wa maji.

Kazi na Majukumu ya Ofisi za Bonde

Maji juu ya ardhi

 •  Kusimamia mtandao wa vituo vya kupimia maji
 •  Kuboresha mfumo wa takwimu za maji za bonde
 •  Kutafiti upatikanaji na matumizi ya maji

Maji chini ya ardhi

 • Kutafiti maji yaliyopo chini ya ardhi
 • Kusimamia na kuboresha mfumo wa takwimu za maji chini ya ardhi
 • Kusimamia na kufanya tathmini ya uchimbaji

Mipango ya rasilimali za maji na utafiti

 •  Kufanya tathmini ya rasilimali za maji
 • Kuratibu mipango ya bonde
 •  Kuratibu wadau wa maji

Kusimamia sheria na utunzaji wa mazingira

 •  Kutoa vibali na hati za kutumia maji
 • Kusimamia matumizi, kanuni na taratibu za kutumia maji
 •  Kusajili vyama vya watumia maji
 •  Kuzuia uchafuzi wa vyanzo vya maji na
 • Kuratibu masuala ya mazingira ya vyanzo vya maji ndani ya bonde

Mitandao ya vituo vya kupimia maji

Vituo vya kupimia maji katika bonde vinasimamia mtiririko wa maji kwenye mito, hadi sasa kuna vituo 35 vya kupimia maji, vituo 5 vya hali ya hewa, na kupima kiasi cha mvua.