Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ujenzi wa Bwawa la Kidete kuanza mwaka huu wa fedha

Swahili

Serikali imewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro kuwa ujenzi wa Bwawa la Kidete utaanza kabla ya kufikia ukomo wa bajeti ya fedha ya mwaka 2016/17. Majibu hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mha. Isaack Kamwelwe wakati akijibu swali la Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule kuhusu ujenzi wa bwawa hilo utaanza lini katika Kipindi cha Maswali na Majibu bungeni.

“Ujenzi wa bwawa hili umepewa kipaumbele, kutokana na hatari ya mafuriko yanayotishia maisha ya wakazi wa Kilosa na mali zao. Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imesitisha safari zake kutoka Dar es Salaam, kutokana na sehemu kubwa ya reli katika eneo hilo kung’olewa na mafuriko,” alisema Mha. Kamwelwe. Akijibu swali hilo Naibu Waziri alisema wizara inakamilisha hatua ya upembuzi yakinifu wa mradi huo na itatenga fedha za kukamilisha mradi huo kwa mwaka huu wa fedha.

“Nilitembelea eneo hilo na nilishuhudia umuhimu wa ujenzi wa bwawa hilo, na ninawahakikishia wakazi wa Kilosa ujenzi wake utaanza kabla ya mwaka huu wa fedha wa Serikali kwisha,” alisisitiza Mha. Kamwelwe.

Photo: