Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hotuba

Mheshimiwa Spika, leo hii Bunge lako Tukufu limepokea taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mheshimiwa Daktari Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang’, inayohusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Naomba sasa, kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida na Maendeleo ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2017/2018.

 Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati hiyo kwa kupokea na kuchambua Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2017/2018. Maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji yamezingatiwa wakati wa maandalizi ya bajeti ya Wizara yangu.

 Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daktari John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa uongozi makini na thabiti waliouonesha katika mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na juhudi zao kwenye ukusanyaji wa kodi; kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali; pamoja na mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, na madawa ya kulevya. Vilevile, nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi hao kwa azma yao ya dhati ya kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda. Hii ni ishara tosha ya uzalendo walionao kwa nchi yetu na imani yao katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo ya haraka na ya uhakika.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Hotuba Bonyeza HAPA