Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taarifa kwa vyombo vya Habari

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Gerson Hosea Lwenge (Mb), kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Sheria ya DAWASA ya mwaka 2001, amemteua  Mhandisi  Romanus Attilio Mwang’ingo kuwa Kaimu  Afisa  Mtendaji  Mkuu  wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Majitaka Dar es Salaam (DAWASA). Uteuzi huo  unaanza mara moja.   Kabla ya uteuzi  huu,  Mhandisi Romanus Attilio Mwang’ingo alikuwa Mkurugenzi Huduma za Ufundi  wa DAWASA

Kwa Maelezo zaidi bonyeza HAPA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi zimekubaliana kuanzisha Kamisheni ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe. Makubaliano hayo yalitiwa saini kati ya Mawaziri wanaohusika na Maji na Umwagiliaji katika mkutano wa wawekezaji wa kuendeleza bonde hilo uliofanyika wiki iliyopita jijini Lilongwe, nchini Malawi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Bingu. 

Kongamano hili lililenga kuwashawishi wawekezaji na washirika wa maendeleo kuwekeza na kufadhili miradi itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 ya Awamu ya Tatu ya Programu ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe kuanzia mwaka 2017 inayokadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 829.  

Makubaliano ya kuanzisha kamisheni yalitiwa saini na Mawaziri wanaohusika na masuala ya Maji na Umwagiliaji wa nchi hizi. Mawaziri hao ni Mhe. Mhandisi Gerson H. Lwenge (MB) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Aggrey C. Masi (MB) wa Jamhuri ya Malawi. Tukio hili la kusaini lilishuhudiwa na Prof. Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Tanzania, Mhe. Balozi Victoria Mwakasege, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Bi. Erica Maganga, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Maji, Malawi, pamoja na wadau waliohudhuria kongamano hilo.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika bonde hili ni pamoja na ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme (megawati 180.2), kilimo cha umwagiliaji, (hekta 6,200) usambazaji wa maji kwa wananchi, ujenzi wa miundombinu ya jamii (bararabara, shule, na vituo vya afya). Miradi mingine ni uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, uvuvi, utalii na uboreshaji wa mazingira, hususan kuimarisha kingo za mto ambao ni mpaka wa nchi zetu mbili.