Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mhandisi Nguli wa Wizara ya Maji apata ajali, Anusurika Kifo

Mhandisi Mwandamizi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Goyagoya Mbenna amepata ajali ya gari eneo la Nanganga, Wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara akiwa safarini kuelekea Songea, mkoani Ruvuma siku ya Jumatano, Agosti 23, majira ya saa tisa alasiri.

Inj. Goyagoya alikuwa akielekea Songea, mkoani Ruvuma kufuatilia taarifa zake za kiutumishi kwa ajili ya kuziwakilisha Utumishi kwa ajili ya taratibu za kustaafu, alikumbana na ajali hiyo mara baada ya tairi la gari alilokuwa akiendesha kupasuka mwendo mfupi kabla ya kufikia tuta lililokuwa mbele yake barabarani.

Mara baada ya ajali hiyo alipelekwa kwenye Hospitali ya Ndanda, mkoani Mtwara na kugundulika kuwa amepata maumivu ya mkono na mbavu, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi, ambapo hali yake inaendelea vizuri kwa sasa.

Inj. Goyagoya ni moja ya wahandisi wenye uzoefu mkubwa wizarani kwenye Idara ya Maji Vijijini, hususani katika usanifu wa miradi ya maji pamoja na maswala ya umeme, pia ameshiriki katika kufanya usanifu wa miradi mbalimbali ya maji vijijini nchini, ukiwemo mradi wa maji wa Ichwankima-Imalabupena unaotekelezwa sasa kwenye Wilaya ya Chato, mkoani Geita.

Mradi huo utahudumia vijiji kumi na moja (11) vya Ichwankima, Nyamirembe, Kalebezo, Nyambiti, Busalala, Kachwamba, Mwangaza, Igalula, Idogelo, Ipandikilo na Imalabupina.

Mara baada ya taarifa za ajali kufika wizarani, watumishi mbalimbali wa Sekta ya Maji walianza kutoa michango kwa ajili ya kumsaidia, ambapo namba maalum ya kukusanyia michango ilitolewa na zaidi ya kiasi cha Sh. mil 7 zimeshakusanywa kwa ajili ya kumsaidia Inj. Goyagoya.