Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Magufuli aweka Mawe ya Msingi Ujenzi wa Miradi ya Maji na Kufungua Miradi iliyokamilika Kigoma na Tabora

Swahili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua na kuweka mawe ya mzingi katika miradi ya maji Mkoani Kigoma na Tabora. Mkoani Tabora, mradi utahusu upanuzi wa mtandao wa maji kutoka ziwa Viktoria kwenda miji ya Tabora, Igunga na Nzega.  Akihutubia wakazi wa Tabora waliofika kwenye sherehe za uwekaji jiwe la msingi Rais Magufuli alisema, ziwa Viktoria ni zawadi aliyotujaalia mwenyezi Mungu hivyo ni lazima tulitumie katika kuwapatia maji wananchi ambao hawana vyanzo vya uhakika vya maji. Pia Rais amewaahidi wakazi wa Tabora, Igunga, Nzega na maeneo ya jirani ya bomba kuwa baada ya miezi 30 shida ya maji itakuwa historia.

Mradi huu, ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Serikali wa kufikisha maji ya Ziwa Victoria katika maeneo mbalimbali ya kanda hii, ambayo hayana vyanzo vya uhakika vya maji.  Akimkaribisha Mhe. Rais, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge alisema Mradi huu unajengwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India kupitia Benki ya EXIM kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 268.35. Usanifu wa Mradi na uandaaji wa makabrasha ya zabuni za ujenzi ulifanywa na Kampuni ya WAPCOS Ltd ya India ambao ndiyo wasimamizi wa mradi huu na yalikamilika mwezi Desemba 2015. Ujenzi Mradi umegawanywa katika sehemu tatu na kila sehemu itakuwa na Mkandarasi wake. Sehemu ya kwanza itaanzia Kijiji cha Solwa (kilichopo Wilaya ya Shinyanga Vijijini) hadi Mji wa Nzega. Ujenzi wa sehemu hii utafanywa na Kampuni ya Megha Engineering Infrastructures Ltd ya India.

Sehemu ya Pili inaanzia Mjini Nzega hadi katika Manispaa ya Tabora kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Ujenzi wa Sehemu hii utafanywa na Kampuni ya L&T ikishirikiana na Kampuni ya Shriram zote kutoka India. Sehemu ya tatu inaanzia Nzega Mjini hadi Igunga Mjini, ujenzi utafanywa na Kampuni ya Afcons ikishirikiana na Kampuni ya SMC zote kutoka India.  Mikataba ya ujenzi wa Mradi ilisainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo na Makandarasi wa ujenzi huo tarehe 22 Aprili 2017 na shughuli za ujenzi zimeanza baada ya Wakandarasi kufanya sehemu kubwa ya maandalizi. Kwa mujibu wa Mikataba hiyo, ujenzi wa Mradi wote unatarajiwa kuchukua jumla ya miezi therathini (30). Mradi huu pia utapeleka maji mji wa Tinde. Aidha, Mji wa Sikonge umepangwa kuunganishwa kwenye mtandao wa maji ya Ziwa Victoria katika mpango wa fedha za mkopo wenye masharti nafuu wa Dola milioni 500  za Marekani kutoka Serikali ya India.

Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia upatikanaji wa maji safi na salama hadi kufikia asilimia 100 katika Manispaa ya Tabora na Miji ya Igunga, Nzega, Uyui pamoja na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, mbapo jumla ya wakazi wanaokadiriwa kufikia milioni moja watakuwa na uhakika wa kupata huduma ya maji safi na salama pamoja na mifugo yao. Akiwa Mkoani Kigoma Waziri wa maji na Umwagiliaji amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na miundombinu ya maji ili miradi inayojengwa iwe endelevu na kuhudumia wakazi wa sasa na vizazi vijavyo.

Photo: