Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Matukio

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA) ifanye bidii na kuhakikisha Mtwara inapata maji kwa asilimia 100, ikizingatiwa ni mji ulio na viwanda vikubwa, ili kuunga mkono Sera ya Viwanda inayotekelezwa na Serikali.

Prof. Mkumbo alisema hayo katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya mkoani Mtwara, alipokuwa akitembelea mamlaka hiyo kwa nia ya kujua utendaji kazi wake na mipango ya utekelezaji wa miradi yake.

“MTUWASA imeshika nafasi ya 8 kati ya mamlaka 25 nchini mwaka huu kulingana na ripoti ya EWURA, ni moja ya mamlaka zinazofanya vizuri. Hivyo, hamna budi kutoka asilimia 60 ya huduma mnayotoa sasa na kufikisha asilimia 100, ili kuendana na mahitaji ya wananchi pamoja na viwanda vikubwa vilivyopo mjini hapa”, alisema Katibu Mkuu.

 Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa ili kuendana na Sera ya Viwanda huduma ya maji haina budi kuwa ya uhakika na endelevu, na MTUWASA inabidi wahakikishe Serikali inafanikiwa kufikia lengo hilo kama watoa huduma wa maji.

Aidha, aliwaasa wananchi wa Mtwara kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji, kwani pamoja na juhudi za Serikali za kuwekeza katika miradi mikubwa ya maji, itakuwa ngumu kufanikisha lengo la kutoa huduma ya uhakika na endelevu ya majisafi na salama kama vyanzo vya maji havitatunzwa na kuwa endelevu.

Naye Mkuregenzi Mtendaji wa Mamlaka ya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA), Inj. Mashaka Sitta alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha mamlaka hiyo inakuwa bora nchini ndani ya miaka miwili; baadhi ya mipango yao ikiwa ni kutunza vyanzo vya maji, kuongeza mitandao ya miundombinu ya maji, kuongeza uzalishaji na wateja ili kufikia lengo hilo.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu alitembelea pia Ofisi za Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini na kukutana na baadhi ya watendaji wake na kuzungumza nao kuhusu usimamizi na maendeleo ya rasilimali za maji katika bonde hilo na kukamilisha ziara yake ya siku mbili katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Ng’apa uliopo mkoani Lindi, mara baada ya ziara aliyoifanya mjini Lindi. Prof. Mkumbo amefanya ziara hiyo kwa nia ya kujua hali ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa, ambao unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya mji wa Lindi (LUWASA), kama sehemu ya kufuatilia maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais John Magufuli miezi michache iliyopita wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

“Hali ya huduma ya maji Lindi si nzuri, ukizingatia inakidhi asilimia 40 tu ya mahitaji. Kwa mradi huu wa Ng’apa ukikamilika utatoa huduma ya maji kwa asilimia 100 kwa wakazi wa mji wa Lindi, ikumbukwe Mhe. Rais alifanya ziara Lindi na akatoa maelekezo kuhusu mradi huu”, alisema Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo alisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais na amefurahishwa na maendeleo ya mradi huo, na kuwa maji yameshafika na kilichobaki ni kupelekwa kwenye chujio ambalo lipo kwenye matengenezo kabla ya kuanza kusambazwa kwa wananchi. Huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na LUWASA haina budi kutekeleza mradi huo kwa wakati kwa niaba ya Serikali.

Wakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (LUWASA), Inj. Riziki Chambuso alisema mradi huo umefikia hatua nzuri na watatekeleza agizo la Rais kuwa ifikapo mwezi Julai mradi utakuwa umekamilika na kuwapatia wakazi wa Lindi mjini maji. Mradi wa Ng’apa ni moja ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kama sehemu ya ahadi yake na unategemea kugharimu Sh. bilioni 29, kufikia sasa Sh. bilioni 22 zimeshatolewa. Ujenzi wa mradi huo, pia utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu hiyo kwa ajili ya kusambazia maji.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi zimekubaliana kuanzisha Kamisheni ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe. Makubaliano hayo yalitiwa saini kati ya Mawaziri wanaohusika na Maji na Umwagiliaji katika mkutano wa wawekezaji wa kuendeleza bonde hilo uliofanyika wiki iliyopita jijini Lilongwe, nchini Malawi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Bingu. 

Kongamano hili lililenga kuwashawishi wawekezaji na washirika wa maendeleo kuwekeza na kufadhili miradi itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 ya Awamu ya Tatu ya Programu ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe kuanzia mwaka 2017 inayokadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 829.  

Makubaliano ya kuanzisha kamisheni yalitiwa saini na Mawaziri wanaohusika na masuala ya Maji na Umwagiliaji wa nchi hizi. Mawaziri hao ni Mhe. Mhandisi Gerson H. Lwenge (MB) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Aggrey C. Masi (MB) wa Jamhuri ya Malawi. Tukio hili la kusaini lilishuhudiwa na Prof. Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Tanzania, Mhe. Balozi Victoria Mwakasege, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Bi. Erica Maganga, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Maji, Malawi, pamoja na wadau waliohudhuria kongamano hilo.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika bonde hili ni pamoja na ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme (megawati 180.2), kilimo cha umwagiliaji, (hekta 6,200) usambazaji wa maji kwa wananchi, ujenzi wa miundombinu ya jamii (bararabara, shule, na vituo vya afya). Miradi mingine ni uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, uvuvi, utalii na uboreshaji wa mazingira, hususan kuimarisha kingo za mto ambao ni mpaka wa nchi zetu mbili.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ametembelea Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu na kujionea uzalishaji wa maji unavyofanyika katika eneo la Mlandizi, Kibaha, mkoani Pwani.

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika mtambo huu wa Ruvu Juu, hatuna budi kuitunza miundombinu yetu ili kuleta tija ya uwekezaji huu mkubwa. Tutumie maji vizuri na kwa matumizi ya msingi, ili tuepukane na tatizo la upotevu wa maji”, alisema Prof. Mkumbo. Katibu Mkuu alimuagiza Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Cyprian Luhemeja kuchukua hatua kwa Mameneja wa Ofisi za Kanda za DAWASCO kwa kuwapa uwiano sawa wa maji, na kuwapima utendaji wao wa kazi kwa kiasi cha maji wanayoyauza na yanayopotea kwa kuleta ufanisi wa kazi yao ili kuhakikisha tatizo la maji Dar es Salaam linatatuliwa.

Aidha, alidhirika na juhudi zinazofanywa katika kuleta suluhisho la upatikanaji wa maji ya uhakika jijini Dar na kuongeza Serikali imejipanga kufikisha maji katika maeneo yasiyo na miundombinu ya maji, hasa ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa maji umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Hivyo, wanafanya utaratibu wa kuwekeza katika hilo ili kuwapa wananchi huduma bora ya majisafi na salama.

Ziara hiyo ni ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo, ambayo aliambatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, watendaji wa DAWASCO na DAWASA na watumishi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mtambo wa maji wa Ruvu Juu kwa sasa unazalisha maji lita milioni 196 kwa siku, kutoka lita milioni 82 zilizokuwa zikizalishwa awali, baada ya kazi ya kuunganisha umeme kukamilika Aprili 15, mwaka huu na kuwasha pampu kubwa mpya ya majisafi na majitaka.

Upanuzi wa mtambo huo na ulazaji wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara uligharimu Dola za kimarekani mil 99 kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India.

Katibu Mkuu Wizara ya maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo na Visay Uplenchwar wa Kampuni ya Megha Engineering Infrastructures Ltd akisaini Mikataba ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka kijiji cha Solwa Shinyanga na kupeleka maji Nzega.

Tanzania imeshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Mashariki ya Kati na Afrika wa Mazingira “Middle East-Africa Environment Forum” uliofanyika Juni, 8-9 katika Jiji la Seoul, nchini Korea.  Mkutano huo wa kimataifa uliandaliwa na Serikali ya Korea ulilenga kubadilishana maaarifa na uzoefu katika masuala ya utunzaji mazingira na utoaji wa huduma bora ya maji na usafi wa mazingira, pamoja na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya uwekezaji baina ya nchi za Afrika, Mashariki ya Kati na Korea. Katika Mkutano huo, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji chini ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Inj. Emmanuel Kalobelo, ambaye alipata nafasi ya kukutana na kunadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania katika miradi ya maji na umwagiliaji, mbele ya Makamu Waziri wa Mazingira wa Korea, Dkt. Jeong Yeon-man na kubadilishana uzoefu kuhusiana na masuala ya mazingira.

Pia, alifanikiwa kukutana na wawekezaji wa Korea, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na wawakilishi wa nchi mbalimbali kutoka Afrika na Mashariki ya Kati zikiwemo Zambia, Kenya, Iran, Burkina Faso, Misri na Msumbiji. Inj. Kalobelo alipata nafasi ya kuonyesha fursa zilizopo nchini Tanzania wakati akiwasilisha mada yake katika mkutano huo, na kuzivutia Serikali ya Korea pamoja na Sekta zake Binafsi kwa fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta za Maji na Umwagiliaji, na kukubali kuongeza uwekezaji katika sekta hizo nchini na kuahidi kuzidisha ushirikiano uliopo kati yao na Tanzania. Pamoja na kutoa fursa za mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa wataalamu wa Sekta Mazingira na Maji Tanzania.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu alifanya ziara kwenye makampuni mbalimbali ya Korea ambayo yameonesha nia ya kuwekeza Tanzania, kwa lengo la kubaini uwezo wa makampuni hayo katika kutekeleza miradi mikubwa ya maji na umwagiliaji ili kupata uhakika wa uwezo wa makampuni hayo katika uwekezaji huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo amezungumza kwa mara ya kwanza na watumishi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji walio katika Ofisi za Dar es Salaam tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Dhumuni la kikao hicho lilikuwa ni kujitambulisha rasmi kwa watumishi hao na kuwapa mikakati yake katika kutekeleza majukumu ya wizara, ili kufikia malengo ya kuwapa wananchi huduma ya uhakika ya majisafi na salama. Akizungumza katika kikao hicho Prof. Mkumbo alisema tumepewa jukumu la kusimamia sekta hii muhimu na Rais anataka kuona matokeo, hivyo hatuna budi kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji iishe kwa wakati na viwango sahihi.

“Wito wangu ni kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maji, iishe kwa wakati na ili tufanikiwe inabidi tuipe msukumo mpya. Tusifanye kazi kwa mazoea na tufanye bidii ili tuweze kufikia lengo kuu, ambalo ni kutoa huduma ya majisafi na salama yanayotosheleza”, alisema Katibu Mkuu. “Ninaahidi kuwapa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza malengo ya Wizara, lakini na mimi pia nahitaji ushirikiano wenu ili tufike tunakotaka kufika. Tuwe na umoja katika jambo hili na ninaamini hatuna sababu ya kushindwa”, alisema Prof. Mkumbo. Wakati huo huo, Mwenyekiti wa TUGHE, Alfred Mashalah alimkaribisha Katibu Mkuu huyo wizarani na kumuahidi ushirikiano wa dhati kwa niaba ya watumishi, na kumtakia kila la heri katika utendaji wake wa kazi.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na watendaji wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara, waliowakilisha taasisi zao.