Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Dkt. Abdel Aty Avutiwa na Mtambo Mpya wa Kusukuma Maji wa Ruvu Chini

Swahili

Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty amevutiwa na mtambo mpya wa kusukuma maji wa Ruvu Chini, mara baada ya kufanya ziara kwenye Mradi wa Maji wa Ruvu Chini uliopo Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani na kujionea mtambo huo uliofungwa hivi karibuni jinsi unavyofanya kazi, akiwa pamoja na mwenyeji wake Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge.

Dkt. Mohamed Abdel Aty alisema kuna maendeleo makubwa ya Sekta ya Maji nchini, na hakika Serikali ya Tanzania inachukua hatua kuhakikisha huduma ya majisafi inaimarika na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na miji ya Kibaha na Bagamoyo. “Serikali ya Tanzania inastahili pongezi kwa uwekezaji huu uliofanywa hapa Ruvu Chini, hii ni hatua kubwa katika kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi. Nimeona fursa nyingi Tanzania, pamoja na kujifunza mengi nina uhakika kupitia ushirikiano wetu, tutafanikiwa kuinua Sekta za Maji na Umwagiliaji Tanzania”, alisema Dkt. Abdel Aty.

Dhumuni la ziara hiyo ilikuwa ni muendelezo wa utaratibu wa kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Misri kwenye maeneo ya maji na umwagiliaji, lengo likiwa ni kuinua sekta hizo katika mataifa hayo kupitia ushirikiano ilionao. Huku Serikali ya Misri ikiwa tayari kutekeleza awamu ya pili ya uchimbaji wa visima 40 kwenye wilaya kame nchini, ambapo awamu ya kwanza ya uchimbaji wa visima 30 vilivyozinduliwa Novemba, mwaka jana katika Wilaya za Same, Mwanga, Kiteto, Bariadi na Itilima. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge ni Rais wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty ni Makamu Rais chini ya mwavuli wa Nile Basin Initiative (NBI), chombo kinachosimamia maendeleo ya rasilimali ya maji ya Mto Nile kwa Nchi 10 wanachama za Afrika.

Photo: