Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bonde la Ziwa Victoria

Bonde la Ziwa Victoria ndani yake kuna Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa kuliko yote Barani Afrika na chanzo cha mto  White Nile. Ziwa Victoria lipo katika Latitudi 031 Kaskazini na 354 Kusini, na Longitudi 3118 Mashariki na 3454 Magharibi.

Lina wastani wa kina cha mita 80. Ziwa hili linajumuisha nchi 3 ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda. Mito ambayo inamwaga maji Ziwa Victoria ni pamoja na Mto Kagera, Simiyu, Mbarageti, Gurumeti, Mara na Mori. Upande wa Mashariki wa bonde hasa katika miinuko ya Tarime, misimu ya mvua ni miwili, wakati upande wa Kusini wa bonde ambao ni mkoa wa Mwanza kuna msimu wa mvua na kiangazi, na upande wa Magharibi unapata mvua kipindi chote cha mwaka na mvua chache katika mwezi wa saba.

Kiasi cha wastani wa mvua kwa mwaka kinatofautiana katika maeneo mbalimbali ya ziwa na maeneo yanayolizunguka. Upande wa Mashariki wastani wa mvua kwa mwaka ni kati ya 500 na 700mm. Upande wa Magharibi mvua huongezeka hadi kufikia wastani 2000mm katika maeneo ya Bukoba na visiwa vya Ssese. Upande wa kusini mwa ziwa katika maeneo ya Mwanza wastani wa mvua ni kati ya 750-1100mm na upande wa Mashariki katika maeneo ya Mara wastani wa mvua kwa mwaka ni kati ya 750-1000mm na huongezeka hadi 1600mm katika miinuko ya Tarime.