Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bonde la Ziwa Tanganyika

Bonde la Ziwa Tanganyika liko Magharibi mwa nchi ya Tanzania, Bonde hili linajumuisha mabonde yote madogo yanayomwaga maji yake katika ziwa Tanganyika. Bonde lina ukubwa wa kilometa za mraba 239,000 na ukubwa wa ziwa lenyewe ni kilometa za mraba 32,000. Eneo la ardhi kwa upande wa Tanzania ni kilometa za mraba 151,000 ni sawa 60% ya maji yanayoingia ziwa Tanganyika. Sehemu kubwa ya bonde ni Mto Malagarasi yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 130,000.

Mto Malagarasi umeanzia katika maeneo ya milima ya mpakani mwa Burundi na Tanzania katika muinuko wa 1750 kutoka usawa wa bahari. Mto unateremka Kaskazini mashariki kupitia kwenye vilima na miteremko kuelekea kwenye ardhi chepechepe ya Malagarasi. Vijito vikuu vya mto Malagarasi ambavyo ni Myowosi na Igombe vinakutana katika Ziwa Nyamagoma. Mito ya Ugala na Ruchungi inakutana na mto Malagarasi upande wa chini wa Ziwa Nyamagoma, Kwa upande wa Magharibi unapita kwenye majabali ya Misito ambapo yanatengeneza maporomoko kabla ya kuingia Ziwa Tanganyika. Mto Ugala unapokea maji kutoka katika eneo la kilometa za mraba zipatazo 52,000 na kabla haujakutana na mto Malagarasi unapita katika maeneo oevu na kutengeneza Ziwa la muda la Ugala na Sagara.

Vijito vingine vikubwa ni Ruchungi unaopokea maji kutoka vilima vya kaskazini vya Kasulu kuelekea upande wa kusini na kupitia katika maeneo oevu kabla ya kuingia mto Malagarasi maeneo ya Uvinza. Pamoja na mto Malagarasi Ziwa Tanganyika pia linapokea maji kutoka katika mabonde madogo madogo, upande wa kaskazini Magharibi wa Kigoma kuna mto Luiche, ambao hufurika wakati wa mvua.