Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bonde la Mto Rufiji

Ofisi ya Maji Bonde la Rufiji inayosimamia matumizi ya maji katika Bonde la Rufiji. Bonde hili maana yake ni eneo lote ambalo mwelekeo wa maji yake huingia Mto Rufiji na hatimaye Bahari ya Hindi. Bonde hilo lina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 177,420 na lina mito mikuu minne ambayo ni Great Ruaha Mkuu wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 82,970, Kilombero wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 39,990. Mto mwingine ni Luwegu wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 26,300 na Mto Rufiji wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 22,160.

Ofisi ya Bonde la Rufiji iko katika Mkoa wa Iringa barabara ya Dodoma. Kimuundo ofisi hiyo iko chini ya Idara ya Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji. Hutekeleza malengo yake kwa kushirikiana na ofisi za Halmashauri za Wilaya zote zilizoko kwenye Bonde hilo. Bonde hilo lina Bodi yake ambayo ina wajumbe kumi ambapo Afisa Maji wa Bonde ndiye Katibu wa Bodi hiyo. Bodi na ofisi ya Bonde la Rufiji ilianzishwa Septemba 1993, kwa mujibu wa Sheria ya Maji Na.42 ya mwaka 1974 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1981 na 1991. Aidha, Waziri mwenye dhamana ya rasilimali za maji ndiye mteuzi wa Bodi hiyo.